Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Hawza, kitabu cha Mijadala 101 ya Kuvutia na Kusisimua, kilichoandikwa na Muhammad Muhammadi Ishtihardi, kimekusanya mijadala mbalimbali inayohusu masuala ya kiitikadi na kidini, tovuti ya Shirika la Habari la Hawza, itakuwa ikikichapisha kitabu hicho katika matoleo mbalimbali.
Mjadala wa Imam Ridha (as) na mmoja wa watu waliomkanusha Mwenyezi Mungu
Mtu mmoja aliekuwa akimkanusha Mwenyezi Mungu alifika mbele ya Imam Ridha (as). Wakati huo, kulikuwa na kundi la watu waliokuwepo katika kikao cha Imam (as). Imam akamwambia yeye:
«Ikiwa haki itakuwa upande wenu, jambo ambalo kwa hakika sivyo, basi katika hali hiyo, sisi na nyinyi tutakuwa sawa, na swala zetu, saumu zetu, zaka zetu na imani yetu havitatuletea madhara yoyote. Lakini ikiwa haki itakuwa upande wetu, kama ilivyo kweli, basi sisi tutakuwa wenye kufuzu na kuokoka, ilhali nyinyi mtakuwa wenye hasara na kuangamia.»
Mtu aliyemkanusha Mwenyezi Mungu: Niambie, Mwenyezi Mungu ana sura na hali gani, na yuko wapi?
Imam Ridha (as):
«Ole wako! Njia unayoifuata si sahihi. Mwenyezi Mungu aliumba dhana ya “jinsi” na hali, bila ya Yeye mwenyewe kuwa na sifa ya jinsi au hali yoyote; na akaumba “mahali”, bila ya Yeye mwenyewe kuwa na mahali.
Kwa hiyo, Dhati takatifu ya Mwenyezi Mungu haitambuliki kwa jinsi wala kwa mahali; hawezi kutambuliwa kwa kutumia nguvu zozote za milango ya fahamu, wala hafanani na kitu chochote.»
Mtu aliyemkanusha Mwenyezi Mungu: Ikiwa Mwenyezi Mungu hatambuliwi kwa kutumia milango yoyote ya fahamu, basi Yeye si kitu chochote.
Imam Ridha (as):
«Ole wako! Kwa sababu tu milango yako ya fahamu imeshindwa kumtambua, unamkanusha? Hali ya kuwa sisi, licha ya milango yetu ya fahamu pia kushindwa kutambua Dhati yake takatifu, tunamuamini na tuna yakini kwamba Yeye ndiye Mola wetu, na kwamba hafanani na kitu chochote.»
Mtu aliyemkanusha Mwenyezi Mungu: Niambie, Mwenyezi Mungu amekuwepo tangu wakati gani?
Imam Ridha (as):
«Niambie, Mwenyezi Mungu hakuwepo tangu wakati gani, ili nami nikuambie amekuwepo tangu wakati gani.»
Mtu aliyemkanusha Mwenyezi Mungu: Ni hoja gani inayothibitisha uwepo wa Mwenyezi Mungu?
Imam Ridha (as):
«Ninapoutazama mwili wangu, ninaona kwamba siwezi kuongeza wala kupunguza chochote katika urefu wake wala upana wake. Siwezi kuondoa madhara na mabaya yaliyomo ndani yake, wala siwezi kuuletea manufaa yoyote.
Kutokana na hali hiyo, nilipata yakini kwamba jengo hili lina mjenzi wake, na nikakiri uwepo wa Muumba.
Zaidi ya hayo, mzunguko wa sayari, kutokea mawingu, kuvuma upepo, pamoja na mwendo wa jua, mwezi na nyota, yote hayo ni alama zinazoonesha kwamba vitu hivi vinavyozunguka vina Mwendeshaji anayevizungusha, na kwamba viumbe hivi vina Muumba na Msimamizi anayeviongoza na kuendesha mambo yake.»¹
Rejea:
¹. Usul al-Kafi, Juzuu ya 1, uk. 78.
Maoni yako